Ijumaa, 8 Februari 2019

Matamshi ya Mungu | “Namna ya Kujua Tabia ya Mungu na Matokeo ya Kazi Yake” Sehemu ya Tatu

Matamshi ya Mungu | “Namna ya Kujua Tabia ya Mungu na Matokeo ya Kazi Yake” Sehemu ya Tatu

Namna Ambavyo Mungu Huanzisha Matokeo Ya Binadamu na Kiwango Ambacho Hutumia Kuasisi Matokeo ya Binadamu

Kabla ya kuwa na mitazamo au hitimisho zako binafsi, unafaa kwanza kuelewa mwelekeo wa Mungu kwako, kile ambacho Mungu anafikiria, na kuamua kama kufikiria kwako ni sahihi au la. Mungu hajawahi kutumia vipimo vya muda katika kuasisi matokeo ya mtu, na Hajawahi kutumia kiwango cha mateso yaliyovumiliwa na mtu katika kuasisi matokeo yake.
Basi Mungu hutumia kiwango gani katika kuasisi matokeo ya binadamu? Kutumia vipimo vya muda katika kuasisi matokeo ya binadamu—hii ndiyo inaingiliana zaidi na dhana za watu. Na pia kuna hao watu binafsi ambao mara nyingi mnawaona, wale ambao katika wakati fulani walijitolea kabisa, wakatumia muda mwingi kabisa, wakagharamika kabisa, wakateseka kabisa. Hawa ndio, kwa maoni yenu, wanaweza kuokolewa na Mungu. Kile tu ambacho watu hawa wanaonyesha, yote wanayoishi kwa kudhihirisha, ndiyo hasa dhana ya wanadamu kuhusu kiwango ambacho Mungu anaanzisha kuhusiana na matokeo ya binadamu. Bila kujali ni nini unachosadiki, Sitaorodhesha mifano hii mmoja baada ya mwingine. Nikiongea kwa ujumla, mradi tu si kiwango cha kufikiria binafsi kwa Mungu, basi kinakuja kutoka kwenye kufikiria kwa binadamu na ni dhana tu ya binadamu. Ni nini athari za kusisitiza bila mwelekeo dhana na kufikiria kwako binafsi? Bila shaka, athari inaweza kuwa tu Mungu akikusukuma mbali. Hii ni kwa sababu siku zote unaringa kuhusu sifa zako mbele ya Mungu, unashindana na Mungu, na kuleta mzozo dhidi ya Mungu, na hujaribu hata kufahamu kwa kweli kufikiria kwa Mungu, wala hujaribu kuzifahamu nia za Mungu na mwelekeo wa Mungu kwa binadamu. Kuendelea mbele hivi ni kujiheshimu kuliko yote na wala si kumheshimu Mungu. Unajisadiki; husadiki Mungu. Mungu hataki mtu wa aina hii, na Mungu hatamwokoa mtu wa aina hii. Kama huwezi kuachilia aina hii ya mtazamo, na kisha kuirekebisha mitazamo hii ya kale isiyokuwa sahihi; kama ungeweza kuendelea mbele kulingana na maagizo ya Mungu; anza kutenda njia ya kumcha Mungu na kujiepusha na maovu kwa sasa na kusonga mbele; kuweza kuheshimu Mungu na kumwona kuwa mkubwa katika mambo yote; usitumie ndoto zako za kibinafsi, mitazamo au imani katika kujifafanua, kumfafanua Mungu. Na badala yake, unazitafuta nia za Mungu kwa hali zote, unatimiza utambuzi na uelewa wa mwelekeo wa Mungu kwa binadamu, na unatumia kiwango cha Mungu kutosheleza Mungu—kufanya hivi kungependeza! Huku kungemaanisha karibu unaanza katika njia ya kumcha Mungu na kujiepusha na maovu.

Kwa sababu Mungu hatumii namna ambavyo watu hufikiria kwa njia hii au njia ile mawazo na mitazamo yao, kama kiwango cha kuanzisha matokeo ya binadamu, basi ni aina ipi ya kiwango Anayoitumia? Mungu hutumia majaribio kuanzisha matokeo ya binadamu. Kunavyo viwango viwili vya kutumia katika majaribio yanayoasisi matokeo ya binadamu: Kiwango cha kwanza ni idadi ya majaribio ambayo watu hao wanapitia, na kiwango cha pili ni matokeo ya watu hawa katika majaribu haya. Ni viashirio hivi viwili vinavyoasisi matokeo ya binadamu. Sasa tutaweza kufafanua viwango hivi viwili.

Kwanza kabisa, unapokabiliwa na jaribio kutoka kwa Mungu (kidokezo: Inawezekana kwamba katika macho yako jaribio hili ni dogo sana na halifai kutajwa), Mungu atakufanya kuwa na ufahamu kabisa kwamba huu ni mkono wa Mungu juu yako, na kwamba ni Mungu ambaye amepangilia hali hizi zote kwako. Wakati kimo chako hakijakomaa, Mungu atapanga majaribio ili kuweza kukupima. Majaribio haya yatalingana na kimo chako, yale ambayo unaweza kuelewa, na yale ambayo unaweza kustahimili. Kujaribu sehemu yako gani? Kujaribu mwelekeo wako kwa Mungu. Je, mwelekeo huu ni muhimu sana? Bila shaka ni muhimu! Zaidi ya hayo, ni muhimu hasa! Kwa sababu mwelekeo huu wa binadamu ndiyo matokeo anayotaka Mungu, ndicho kitu muhimu zaidi kulingana na Mungu. Ama sivyo Mungu asingetumia jitihada Zake kwa watu kwa kujihusisha na aina hizi za kazi. Mungu hutaka kuuona mwelekeo wako kwake Yeye, kupitia kwa majaribio haya; Anataka kujua kama uko kwenye njia sahihi na Anataka kujua kama unamcha Mungu na kujiepusha na maovu. Hivyo basi, bila kujali kama unaelewa ukweli mwingi au kidogo wakati huo, bado utakabiliwa na majaribio ya Mungu, na kufuatia ongezeko lolote katika kiwango chochote cha ukweli unaouelewa, Mungu ataendelea kupangilia majaribio sawa na hayo kwako. Wakati unapokabiliwa kwa mara nyingine tena na jaribio, Mungu anataka kuona iwapo mtazamo wako, mawazo yako, na mwelekeo wako kwa Mungu umekuwa na ukuaji wowote mpaka sasa. Baadhi ya watu husema: “Kwa nini siku zote Mungu anataka kuiona mielekeo ya watu? Kwani Mungu hajaona namna wanavyouweka ukweli katika matendo? Kwa nini Atake tena kuiona mielekeo ya watu?” Huku ni kupayuka kwa upuuzi! Kwa sababu Mungu anaendelea hivi, basi nia za Mungu lazima ziwe mumohumo. Siku zote Mungu huwaangalia watu kutoka pembeni mwao, akiangalia kila neno na tendo lao, kila kitendo na kusonga kwao, na hata kila fikira na wazo lao. Kila kitu kinachowafanyikia watu: vitendo vyao vizuri, makosa yao, dhambi zao, na hata kuasi na kusaliti kwao, Mungu atazirekodi zote kama ithibati katika kuasisi matokeo yao. Kwa kadri kazi ya Mungu inavyoendelea kuimarika hatua kwa hatua, unasikia ukweli zaidi na zaidi, unakubali mambo mazuri zaidi na zaidi, taarifa nzuri, na uhalisia wa kweli. Kwenye mkondo wa mchakato huu, mahitaji ya Mungu kwako wewe yataongezeka pia. Wakati uo huo, Mungu atapanga majaribio makubwa zaidi kwako. Shabaha yake ni kuchunguza kama mwelekeo wako kwa Mungu umekomaa mpaka sasa. Bila shaka, kwenye kipindi hiki, mtazamo ambao Mungu anahitaji kwako unaingiliana na uelewa wako wa uhalisia wako wa ukweli.

Huku kimo chako kinapoendelea kuimarika kwa utaratibu, kile kiwango ambacho Mungu anahitaji kutoka kwako wewe kitaendelea kuimarika kwa utaratibu pia. Kama utakuwa hujakomaa, Mungu atakupa kiwango kidogo sana; wakati kimo chako kitakapokuwa kikubwa kidogo, Mungu atakupa kiwango cha juu zaidi kidogo. Lakini Mungu atakuwa vipi baada ya wewe kuuelewa ukweli wote? Mungu atahakikisha kuwa unakabiliana na hata majaribio makubwa zaidi. Katikati ya majaribio haya, kile Mungu anachotaka kupata, kile Mungu anachotaka kuona, ni maarifa yako ya kina zaidi ya Mungu na kumcha kwako Kwake kwa njia ya kweli. Wakati huu, mahitaji ya Mungu kwako wewe yatakuwa ya juu zaidi “makali zaidi” kuliko wakati ambapo kimo chako kilikuwa kidogo zaidi (kidokezo: Watu huona kwamba hali hii ni kali, lakini Mungu kwa hakika Huiona kuwa ya kustahimilika). Wakati Mungu anawapa watu majaribio, ni uhalisia gani ambao Mungu anataka kuunda? Mungu anauliza kila mara kwamba watu wampe Yeye moyo wao. Baadhi ya watu watasema: “Mtu anawezaje kufanya hivyo? Natekeleza wajibu wangu, niliacha nyumba yangu na riziki yangu, niligharamika kwa sababu ya Mungu. Hii yote si mifano ya kuutoa moyo wangu kwa Mungu? Ni vipi vingine nitakavyoutoa moyo wangu kwa Mungu? Yaweza kuwa kwamba, hii si mifano ya kuutoa moyo wangu kwa Mungu? Mahitaji mahususi ya Mungu ni yapi?” Mahitaji haya ni mepesi mno. Kwa hakika, kunao baadhi ya watu ambao tayari wameitoa mioyo yao kwa Mungu katika viwango tofauti na awamu mbalimbali za majaribio yao. Lakini wengi wa watu huwa hawapi Mungu mioyo yao. Wakati Mungu anapokupa jaribio, Mungu hutaka kujua kama moyo wako uko pamoja Naye, pamoja na mwili au pamoja na Shetani. Wakati Mungu anapokupa jaribio, Mungu anataka kujua kama unasimama katika upinzani na Yeye au kama unasimama katika hali ambayo inalingana na Yeye, na kutaka kuona moyo wako kama uko na Yeye. Wakati hujakomaa na wakati wa kukabiliwa na majaribio, kiwango cha imani yako kiko chini, na huwezi kujua hasa ni nini unachohitaji ili kutosheleza nia za Mungu kwa sababu unao uelewa finyu wa ukweli. Licha ya haya yote, bado unaweza kumwomba Mungu kwa dhati na uaminifu, kuwa radhi kuutoa moyo wako kwa Mungu, kumfanya Mungu kuwa mkuu wako, na kuwa radhi kumpa Mungu yale mambo unayosadiki kuwa yenye thamani zaidi. Hii ndiyo maana ya wewe kuwa tayari umempa Mungu moyo wako. Unaposikiliza mahubiri mengi zaidi na zaidi, na kuelewa ukweli zaidi na zaidi kimo chako kitaanza kukomaa kwa utaratibu. Kiwango ambacho Mungu huhitaji kutoka kwako si sawa na kile ambacho ulikuwemo wakati ulikuwa hujakomaa; Anahitaji kiwango cha juu zaidi kuliko hicho. Wakati moyo wa binadamu unapewa Mungu kwa utaratibu, unaanza kuwa karibu zaidi na karibu zaidi na Mungu; wakati binadamu anaweza kuwa karibu na Mungu kweli, wanaanza kuwa na moyo ambao sanasana unamcha Yeye. Mungu anataka aina hii ya moyo.

Wakati Mungu anataka kuumiliki moyo wa mtu, Atawapa majaribio mengi. Kwenye majaribio haya, kama Mungu hatauchukua moyo wa mtu huyu, wala Haoni kama mtu huyu anao mwelekeo wowote—hivi ni kusema Havioni vitu ambavyo mtu huyu anapitia au anafanya mambo kwa njia ambayo ni ya kumcha Mungu, na Haoni mwelekeo au suluhisho ambalo linajiepusha na maovu kutoka kwa mtu huyu. Kama hivi ndivyo ilivyo, basi baada ya majaribio mengi, subira ya Mungu kwa mtu huyu binafsi itaondolewa, na Hatamvumilia mtu huyu tena. Hataweza kuwapa watu kama hawa majaribio, na Hataweza tena kuwashughulikia. Basi hiyo inamaanisha kwamba matokeo ya mtu huyu ni yapi? Inamaanisha kwamba hawatakuwa na matokeo. Yawezekana kwamba mtu huyu hajafanya maovu yoyote. Yawezekana pia kwamba watu hawa hawajafanya chochote cha kukatiza au kutatiza. Yawezekana kuwa watu hawa hawajampinga Mungu waziwazi. Hata hivyo, moyo wa mtu huyu umefichwa kutoka kwa Mungu. Hawajawahi kuwa na mwelekeo na mtazamo wazi kwa Mungu, na Mungu hawezi kuona waziwazi kwamba moyo wake amekabidhiwa Yeye, na Yeye Hawezi kuona waziwazi kwamba mtu huyu anatafuta kumcha Mungu na kujiepusha na maovu. Mungu hana subira tena kwa watu hawa, Hatawagharamia tena, Hatatoa tena rehema Yake kwao, na Hatawafanyia kazi wao tena. Maisha ya imani ya mtu huyu katika Mungu tayari hayapo tena. Hii ni kwa sababu katika majaribio yote mengi ambayo Mungu amempa mtu huyu, Mungu hajapata matokeo Anayotaka. Hivyo basi, kunayo idadi ya watu ambao ndani yao Sijawahi kuuona mwangaza na kupata nuru kwa Roho Mtakatifu. Inawezekanaje kuona haya? Mtu wa aina hii huenda aliamini katika Mungu kwa miaka mingi, na kwenye sehemu ya juujuu wamekuwa amilifu. Wamevisoma vitabu vingi, wameyashughulikia masuala mengi, wameandika nakala nyingi, wamekuwa na ujuzi wa barua na falsafa nyingi. Hata hivyo, hakuna ukuaji wowote unaonekana kamwe, na wala kuwa na mtazamo wowote wa kuonekana kwa Mungu kutoka kwa mtu huyu, wala hakuna mwelekeo wowote wazi. Hivi ni kusema kwamba huwezi kuona moyo wa mtu huyu. Moyo wao siku zote umesetiriwa, moyo wao umefumikwa—Umefunikwa kutoka kwa Mungu, hivyo basi Mungu hajauona moyo wa kweli wa mtu huyu, Hajaona kumcha Mungu kwa mtu huyu, na hata zaidi Hajaona namna ambayo mtu huyu anatembea katika njia za Mungu. Kama mpaka sasa Mungu hajampata mtu wa aina hii, Anaweza kuwapata katika siku za usoni? Hawezi! Je, Mungu ataendelea kusukumiza mbele mambo ambayo hayawezi kupatikana? Hatafanya hivyo! Mwelekeo wa Mungu kwa watu kama hawa, hivyo basi ni nini? (Anawasukumia mbali, Hawasikilizi.) Yeye hawasikilizi! Mungu hasikilizi mtu wa aina hii; Anawasukumia mbali. Mmetia kwenye kumbukumbu maneno haya kwa haraka sana, kwa usahihi sana. Inaonekana mmeelewa kile mlichosikia!

Kunao baadhi ya watu ambao, punde wanapoanza kumfuata Mungu wao hawana ukomavu na hawajui chochote; hawaelewi nia za Mungu; hawajui pia maana ya kusadiki Mungu, kuchukua njia iliyoundwa na binadamu na inayokosewa na wengi ya kusadiki Mungu, kufuata Mungu. Wakati mtu wa aina hii anakabiliwa na majaribio hawana habari na hawajali kuhusu mwongozo na nuru ya Mungu. Hawajui maana ya kuutoa moyo wao kwa Mungu na maana ya kusimama imara wakati wa jaribio. Mungu atampa mtu huyu kiwango finyu cha muda na katika kipindi hiki, Atawaacha kuelewa jaribio la Mungu ni nini, na nia za Mungu ni nini. Baadaye mtu huyu atahitaji kuonyesha mtazamo wao. Kuhusiana na watu wale walio katika awamu hii, Mungu angali anasubiri. Kuhusiana na watu wale ambao mitazamo yao ingali inayumbayumba, wale wanaotaka kumpa Mungu mioyo yao lakini hawajawa na maridhiano ya kufanya hivyo, ambao, ingawa wameweza kutenda ukweli fulani, wakati wanapokumbwa na jaribio kuu, wanaokwepa na wanataka kukata tamaa—mwelekeo wa Mungu kwa watu kama hawa ni upi? Mungu angali bado ana matarajio kidogo kwa watu kama hawa. Matokeo yanategemea na mielekeo na utendakazi wao. Mungu anaitikia vipi kama watu si amilifu katika kuwa na maendeleo? Yeye hukata tamaa. Hii ni kwa sababu kabla Mungu hajakata tamaa kwako, tayari wewe mwenyewe umekata tamaa. Kwa hivyo, huwezi kumlaumu Mungu kwa kufanya hivyo, je, unaweza? Je, hiyo ni haki? (Ni haki.)

Swali la Kiutendaji Huleta Aina Zote za Aibu kwa Watu

Kunayo aina nyingine ya mtu aliye na matokeo mabaya zaidi kati ya yote. Hawa ndio Nisiopenda kutaja sana. Hali si mbaya kwa sababu mtu huyu hupokea adhabu ya Mungu, au kwamba mahitaji ya Mungu kwao ni makali na wana matokeo mabaya. Badala yake, hali ni mbaya kwa sababu wanajifanyia wenyewe, kama inavyosemwa mara kwa mara: Wanajichimbia kaburi lao. Mtu kama huyu ni aina gani? Mtu huyu hatembei kwenye njia inayofaa, na matokeo yake yanafichuliwa mapema. Mungu humwona mtu wa aina hii kama lengo Lake kubwa zaidi la chuki Yake. Kama watu wanavyosema hawa ndio wa huzuni kuliko wote. Mtu wa aina hii ni mwenye shauku anapoanza kumfuata Mungu; wanalipia bei nyingi; wanayo maoni mazuri kuhusu mtazamo wa kazi ya Mungu; kufikiria kwao ni kwingi kuhusu mustakabali wao binafsi; wao hasa wanayo imani katika Mungu, wanasadiki kwamba Mungu anaweza kumfanya binadamu kuwa kamili, na kumfanya huyo binadamu kufikia hatima yenye utukufu. Ilhali kwa sababu isiyoeleweka, mtu huyu kisha hukimbia akiwa katika harakati ya kazi ya Mungu. Ni nini maana ya mtu huyu kukimbia? Maana yake ni kwamba wanatoweka bila kwaheri, bila sauti yoyote. Wanaondoka bila kutaja neno lolote. Ingawa mtu wa aina hii anadai kuwa anasadiki Mungu, huwa haweki kamwe mizizi yoyote kwenye njia ya kusadiki Mungu. Hivyo basi, haijalishi ni kwa muda upi wamesadikia, bado wanaweza kumgeuka Mungu. Baadhi ya watu huondoka ili kufanya biashara, baadhi ya watu huondoka ili kuishi maisha yao, baadhi ya watu huondoka ili kutajirika, baadhi ya watu huondoka kuoa au kuolewa, kuwa na watoto…. Miongoni mwa wale wanaondoka, kunao wanaopata shambulizi la nadhari na wanataka kurudi, na wengine wanaoendelea vibaya sana kimaisha, wanaishi maisha tu na kuyasukuma kwa miaka na miaka. Wasukuma maisha hawa wamepitia mateso mengi, na wanasadiki kwamba kuwa ulimwenguni kuna maumivu mno, na hawawezi kutenganishwa na Mungu. Wanataka kurudi nyumba ya Mungu ili kupokea tulizo, amani, furaha, na kuendelea kusadiki katika Mungu ili kukwepa janga, au kuokolewa na kupata hatima nzuri. Hii ni kwa sababu watu hawa wanasadiki kwamba upendo wa Mungu hauna mipaka, kwamba neema ya Mungu haiwezi kuisha na kwamba haiwezi kutumika yote. Wanasadiki kwamba haijalishi ni nini mtu amefanya, Mungu anafaa kumsamehe na kuvumilia maisha yao ya kale. Watu hawa wanasema kwamba wanataka kurudi na kutekeleza wajibu wao. Kuna wale ambao hata wanatoa msaada wa baadhi ya mali yao kwa kanisa, wakitumai kwamba hii ndiyo njia yao ya kurudi katika nyumba ya Mungu. Mwelekeo wa Mungu kwa watu aina hii ni upi? Mungu anafaa kuanzisha vipi matokeo yao? Kuwa huru kuongea. (Ulifikiri kwamba Mungu angewakaribisha watu wa aina hii, lakini baada ya kusikia kwamba sasa hivi, pengine hawatakaribishwa tena.) Na wewe unafikiria vipi? (Mtu wa aina hii huja mbele ya Mungu ili matokeo yao yasije yakawa yale ya kifo. Hawafanyi hivyo kutokana na uaminifu wa kweli. Badala yake, kutokana na maarifa kwamba kazi ya Mungu itakamilika hivi karibuni, wanadanganyika kuwa watapata baraka.) Unasema kwamba mtu huyu kwa kweli hasadiki katika Mungu, na hivyo basi Mungu hawezi kumkubali? Ndivyo ilivyo? (Ndiyo.) (Uelewa wangu ni kwamba mtu wa aina hii ni yule wa kujali maslahi yake kuliko uhaki wa jambo, na kwamba hamsadiki Mungu kwa dhati.) Hajapata kumsadiki Mungu; yeye ni mtu mwenye kuangalia maslahi yake kuliko haki. Yamesemwa vizuri! Watu hawa wanaojali maslahi yao ni wale ambao kila mmoja anawachukia. Wanaenda na mkondo tu, na hawawezi kusumbuliwa ili kufanya kitu isipokuwa kama watafaidi kwa jambo hilo. Bila shaka wanastahili dharau! Je, kati ya ndugu zangu wengine kunaye anayo maoni? (Mungu hatawakubali tena kwa sababu kazi ya Mungu karibu inakamilika na sasa ndipo matokeo ya watu yanaandaliwa. Ni wakati huu ambapo watu hawa wanataka kurudi. Si kwa sababu kwa kweli wanataka kufuata ukweli; wanataka kurudi kwa sababu wanayaona majanga yakishushwa, au wanashawishiwa na mambo ya nje. Kama kweli walikuwa na moyo uliokuwa ukifuatilia ukweli, wasingewahi kukimbia wakiwa katikati ya safari.) Je, yapo maoni mengine? (Hawatakubaliwa. Kwa kweli Mungu aliwapa fursa lakini mwelekeo wao kwake Mungu ulikuwa siku zote kutomsikiliza. Bila kujali nia za mtu huyu ni zipi, na hata kama atatubu, Mungu bado hatamkubali. Hii ni kwa sababu Mungu tayari aliwapa fursa nyingi ajabu ilhali wao walionyesha mtazamo wao: Walitaka kumwacha Mungu. Hivyo basi, watakaporudi sasa, Mungu hatawakaribisha.) (Ninakubali pia kwamba Mungu hatamkaribisha mtu wa aina hii, kwa sababu kama mtu ameona njia ya kweli, akapitia kazi ya Mungu kwa kipindi kirefu kama hicho, na bado anaweza kurudi kwa ulimwengu, kurudi kwa kumbatio la Shetani, basi huu ni usaliti mkuu kwa Mungu. Licha ya hoja kwamba kiini cha Mungu ni rehema, ni upendo, inategemea ni mtu wa aina gani ambaye kiini hicho kinaelekezwa kwake. Kama mtu huyu atakuja mbele ya Mungu akitafuta faraja, kitu cha kuwekea tumaini lake, basi mtu wa aina hii kwa kweli si mtu anayemsadiki Mungu kwa dhati, na rehema za Mungu kwake zinafika hapo.) Kiini halisi cha Mungu ni rehema, kwa hivyo ni kwa nini Hampatii mtu wa aina hii rehema zaidi kidogo tu? Kwa rehema kidogo, hawapati fursa? Awali, mara nyingi ilisemekana: Mungu anamtaka kila mmoja kuokolewa, na hataki mtu yeyote kuangamia. Kama kondoo mmoja miongoni mwa kondoo mia moja atapotea, Mungu atawaacha wale kondoo tisini na tisa kumtafuta yule kondoo aliyepotea. Siku hizi, kuhusiana na mtu wa aina hii, kama ni kwa minajili ya kusadiki kwao kwa Mungu, je, Mungu anafaa kuwakaribisha na kuwapa fursa ya pili? Kwa kweli hilo si swali gumu; ni rahisi mno! Kama kwa kweli mnamtambua Mungu na mnao uelewa halisi wa Mungu, basi hamna ufafanuzi mwingi unaohitajika; hamna kukisia kwingi kunahitajika vilevile, kweli? Majibu yenu yamo katika njia sahihi, lakini bado upo umbali fulani kati yao na mwelekeo wa Mungu.

Sasa hivi tu kulikuwepo na baadhi yenu mliokuwa na hakika kwamba Mungu asingeweza kumkubali mtu wa aina hii. Wengine hawakuwa na hakika sana kuwa Mungu anaweza kuwakubali, na huenda asiwakubali—mwelekeo huu ndio ule wa wastani; na kisha kulikuwa na wale ambao mtazamo wao ulikuwa kwamba wanatumai kwamba Mungu atamkaribisha mtu wa aina hii—huu ndio mwelekeo ule usioeleweka. Wale walio na mwelekeo hakika wanasadiki kuwa Mungu ameshughulika mpaka sasa, na shughuli Yake imekamilika, hivyo basi Mungu hahitaji kuwa mvumilivu na watu hawa, na kwamba Hatawakaribisha tena. Wale watu wa wastani wanasadiki kwamba masuala haya yanafaa kushughulikiwa kulingana na hali inayoyazunguka: Kama moyo wa mtu huyu hauwezi kutenganishwa na wa Mungu, na bado wao ni watu wanaomsadiki Mungu kwa kweli, mtu anayefuatilia ukweli, basi Mungu hafai kukumbuka udhaifu na makosa yao ya awali; Anafaa kuwasamehe, na kuwapa fursa nyingine, kuwaruhusu kurudi katika nyumba ya Mungu, na kukubali wokovu wa Mungu. Hata hivyo, kama mtu huyu atatoroka kwa mara nyingine, hapo ndipo Mungu hatataka mtu huyu na kitendo hiki hakitachukuliwa kuwa cha ukiukaji wa haki. Kunalo kundi jingine ambalo linatumaini kwamba Mungu anaweza kumkaribisha mtu huyu. Kundi hili halina uhakika sana kama Mungu anawakaribisha au la. Kama wanaamini kwamba Mungu anafaa kuwakaribisha, lakini Mungu asiwakaribishe, basi yaonekana kwamba wamepotoka kidogo na mtazamo wa Mungu. Kama watasadiki kwamba Mungu hafai kuwakaribisha, naye Mungu atokee kusema kwamba upendo Wake kwa binadamu hauna kikomo na kwamba Yuko radhi kumpa mtu fursa nyingine, basi huu si mfano wa kutojua kwa binadamu ukimulikwa waziwazi? Kwa vyovyote vile, nyinyi nyote mna mitazamo yenu binafsi. Mitazamo hii ni maarifa katika fikira zenu binafsi; ni onyesho pia ya kina cha uelewa wenu wa kweli na uelewa wenu wa nia za Mungu. Imesemwa vyema, sio? Ni jambo la kupendeza kwamba mnayo maoni katika suala hili! Lakini suala kuhusu kama maoni yenu ni sahihi au si sahihi, kunayo alama ya kiulizo. Je, nyinyi nyote hamna wasiwasi kidogo? “Basi ni gani sahihi? Siwezi kuona vizuri, na sijui hasa kile anachofikiria Mungu. Mungu hakuniambia chochote. Nawezaje kujua anachofikiria Mungu? Mtazamo wa Mungu kwake binadamu ni upendo. Kulingana na mwelekeo wa kale wa Mungu, Anafaa kumkubali mtu huyu. Lakini sina hakika kuhusu mwelekeo wa sasa wa Mungu—ninaweza kusema tu kwamba pengine Atamkaribisha mtu huyu na pengine Hatamkaribisha.” Je, waona vile jambo hili lilivyo la mzaha? Jambo hili limewakoroga. Kama hamna msimamo bora wa suala hili basi ni nini mtakachofanya endapo kanisa lenu litakumbana kwa kweli na mtu wa aina hii? Kama hamtalishughulikia kwa njia bora, basi pengine mtamkosea Mungu. Je, hamuoni kwamba suala hili ni hatari mno?

Kwa nini Ninataka kuulizia maoni yenu kuhusu kile Nilichokuwa Nazungumzia? Nataka kupima mitazamo yenu, kupima ni maarifa kiasi kipi ya Mungu mliyo nayo, ni uelewa kiasi kipi mlio nao katika nia za Mungu na mwelekeo wa Mungu. Jibu ni gani? Jibu limo kwenye mitazamo yenu. Baadhi yenu mnashikilia sana ukale, na baadhi yenu mnatumia kufikiria kwenu katika kukisia. “Kukisia” ni nini? Ni wakati ule ambao hamna wazo lolote namna ambavyo Mungu anafikiria, hivyo basi mnakuja na mawazo yasiyo na msingi kuhusu namna ambavyo Mungu anafaa kufikiria kwa namna hii au namna ile. Hamjui kwa hakika kama kukisia kwenu ni sahihi au si sahihi, na hivyo basi mnatoa mtazamo usioleweka. Mkikumbwa na hoja hii mnaona nini? Wakati wakimfuata Mungu, ni nadra sana kwa watu kutilia maanani makusudi ya Mungu, na wanatilia maanani fikira za Mungu na mwelekeo wa Mungu kwa binadamu kwa nadra sana. Ninyi hamwelewi fikira za Mungu, kwa hivyo mnapoulizwa maswali yanayohusisha nia za Mungu, yanayohusisha tabia ya Mungu, mnaingia katika hali ya kutokuwa na hakika; mnakuwa kwa kweli hamna uhakika, na mnakisia au kubahatisha. Mwelekeo huu ni upi? Unathibitisha hoja hii: Watu wengi wanaomwamini Mungu wanamchukulia kuwa hewa tupu, asiyebainika. Kwa nini Nasema hivyo? Kwa sababu kila wakati mnapokumbwa na suala, hamzijui nia za Mungu. Kwa nini hamzijui? Si kwamba hamzijui tu kwa sasa. Badala yake kuanzia mwanzo hadi mwisho hamjui mwelekeo wa Mungu katika suala hili. Kwenye nyakati zile ambazo huwezi kuona na hujui mwelekeo wa Mungu, umewahi kuutafakaria? Umeutafuta? Umewasiliana ili kuupata? La! Hii inathibitisha hoja: Mungu unayemsadiki na Mungu wa kweli hawajaunganika. Wewe, unayemsadiki Mungu, unafikiria Mungu kuhusu mapenzi yako, unafikiria tu kuhusu mapenzi ya kiongozi wako, na unafikiria tu yale mambo ya juujuu na maana ya kifalsafa ya neno la Mungu, lakini hujaribu kwa kweli kujua na kutafuta mapenzi ya Mungu kamwe. Sivyo ndivyo hali ilivyo? Kiini halisi cha suala hili hakipendezi! Kwa miaka na mikaka Nimeona watu wanaomsadiki Mungu. Kusadiki huku kunachukua mfumo gani? Baadhi ya watu wanasadiki katika Mungu ni kana kwamba Yeye ni hewa tupu. Watu hawa hawana majibu ya maswali kuhusu uwepo wa Mungu kwa sababu hawawezi kuhisi au kuwa na ufahamu uwepo au kutokuwepo kwa Mungu, sikuambii hata kuuona waziwazi au kuuelewa. Kwa nadharia yao, watu hawa wanafikiria kwamba Mungu hayupo. Baadhi wanasadiki katika Mungu ni kana kwamba Yeye ni binadamu. Watu hawa wanasadiki kwamba Mungu hawezi kufanya mambo yale ambayo wao hawawezi kufanya, na kwamba Mungu anafaa kufikiria namna wanavyofikiria. Ufafanuzi wa mtu huyu kuhusu Mungu ni “mtu asiyeonekana na asiyegusika.” Kunalo pia kundi la watu wanaosadiki katika Mungu kana kwamba Yeye ni kikaragosi. Watu hawa wanasadiki kwamba Mungu hana hisia, kwamba Mungu ni sanamu. Wakati wanapokabiliwa na suala, Mungu hana mwelekeo, hana mtazamo, hana mawazo; Anatawaliwa na binadamu. Watu wanasadiki tu wanavyotaka kusadiki. Wakimfanya kuwa mkubwa, Yeye ni mkubwa; wakimfanya kuwa mdogo, Yeye ni mdogo. Wakati wanapotenda dhambi na wanahitaji rehema ya Mungu, wanahitaji uvumilivu wa Mungu, wanahitaji upendo wa Mungu, basi Mungu anafaa kutoa rehema Zake. Watu hao wanafikiria kuhusu Mungu kwenye akili zao binafsi na kumfanya Mungu kutimiza mahitaji yao na kutosheleza matamanio yao yote. Haijalishi ni lini na ni wapi, na haijalishi hata mtu huyu anafanya nini, watakubali mvuto huu katika matendo yao kwa Mungu na kusadiki kwao katika Mungu. Kuna hata wale wanaosadiki katika Mungu kuweza kuwaokoa baada kuikera tabia ya Mungu. Hii ni kwa sababu wanasadiki kuwa upendo wa Mungu hauna mipaka, tabia ya Mungu ni haki, na kwamba bila kujali ni vipi ambavyo watu wanakosea Mungu, Hatakumbuka chochote. Kwa sababu makosa ya binadamu, dhambi za binadamu na kutotii kwa binadamu ni maonyesho ya mara moja ya tabia ya mtu huyo, Mungu atawapatia watu fursa, kuvumilia na kuwa na subira nao. Mungu angali atawapenda kama awali. Kwa hivyo tumaini la wokovu wao lingali kubwa. Kwa hakika, haijalishi ni vipi mtu anavyosadiki Mungu, mradi tu hafuatilii ukweli basi Mungu anashikilia mwelekeo mbaya kwake. Hii ni sababu wakati unamsadiki Mungu, labda unakithamini kile kitabu cha neno la Mungu unakichambua kila siku, unakisoma kila siku, lakini unamweka Mungu halisi pembeni, unamchukulia kama hewa tupu, unamchukulia Yeye kama mtu, na baadhi yenu mnamchukulia kuwa kikaragosi. Kwa nini Nasema hivi? Kwa sababu kutokana na vile Ninavyoona, licha ya kama unakabiliwa na suala au kukumbana na hali, yale mambo yanayopatikana katika nadharia yako, yale mambo ambayo yameimarishwa ndani kwa ndani—hakuna kati ya haya ambayo yana uunganisho wa neno la Mungu au yanafuatilia ukweli. Unajua tu kile wewe mwenyewe unatafuta, maoni yako wewe binafsi, na kisha mawazo yako binafsi, mitazamo yako binafsi inalazimishiwa Mungu. Inakuwa mitazamo ya Mungu, ambayo inatumika kama viwango vya kutii bila kusita. Kwa muda, kuendelea namna hii kunakufanya uwe mbali zaidi na Mungu.




0 评论:

Chapisha Maoni